Ule usemi wa nabii hakubaliki kwao huenda ndiyo unaendana na haya yaliyomtokea mwanamuziki Dayna Nyange baada ya jina lake kutajwa katika tuzo nchini Nigeria.
Nyota huyu amekwepo kwenye fani muda mrefu, na ambaye kwa sasa anavuma na kibao chake cha komela kilichotoka julai mwaka jana na kumshirikisha rapa Billnas, pamoja na kibao hiko na vibao vingine mwanamuziki huyo mkongwe hajawahi kutajwa kuwania tuzo nje ya nchi.
Dayna amefungua pazia la wasanii wa Tanzania kutajwa kwenye tuzo za kimataifa kwa mwaka 2017 za Bravery and Excellence (BAE), zinazofanyika nchini Nigeria.
katika tuzo hizo, Dayna ametajwa kuwania vipengele viwili ambavyo ni Mtumbuizaji Bora wa Afrika na Muimbaji Bora wa Kike.
Kwenye kipengele cha mtumbuizaji bora (Best African Act), Dayna anachuana na Eddy Kenzo (Uganda), Rabbit Kiki kaka (Kenya), Stonebwoy (Ghana) na Jah Vinci (Jamaica).
Upande wa kipengele cha muimbaji bora wa kike (Best African Female Vocal Perfomance), anachuana na Aramide, Ngowari na Rocknana.
Dayna anasema jina lake kutajwa kwenye tuzo ni mafanikio makubwa katika maisha yake hivyo amewaomba watanzania wamuunge mkono kwa kumpigia kura kwa wingi ili tuzo hizo azilete nyumbani.
”kwangu ni kitu kikubwa sana naufungua mwaka 2017 kikazi zaidi, naamini nitashinda kazi imebaki kwa Watanzania ndiyo watakao kamilisha hilo,” alisema Dayna.