Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Kanali Wilson Sakulo amewaagiza maofisa wote wanaohusika na idara ya kutoa vitambulisho vya taifa (NIDA), kuweka utaratibu wa kuwapelekea huduma karibu wananchi wa mipakani, ili kuwaondolea adha ya kusafi ri umbali mrefu.
Kanali Sakulo, ametoa agizo hilo katika kikao cha Baraza la Madiwani la kuhitimisha mwaka wa fedha 2021/2022, huku akithibitisha kupokea malalamiko ya wananchi ya kwenda na kurudi mara kadhaa wilayani kwenye ofisi za NIDA bila mafanikio.
Amesema, sababu kubwa ya kwenda na kurudishwa ni shaka juu ya uraia wao, changamoto itakayoweza kutatuliwa pale watoa huduma watakapokuwa karibu na wananchi hao.
“Wananchi wanakwenda mara nyingi kwa ajili ya kuhojiwa tu kuhusu uraia wao lakini hawapewi huduma wanayohitaji.Kutokana na kukosa vitambulisho au namba ya NIDA kumewakosesha huduma muhimu, ikiwemo kupewa leseni na kuomba nafasi za kushiriki sensa,” amesema