Jamii nchini, imeaswa kutambua na kuthamini mchango unaotolewa na walimu wa Madrasa katika kuwapatia malezi bora watoto wao.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B”, Hamid Seif Said wakati akizungumza na Wazazi, Walimu na Wanafunzi wa Madrasa za Shehia ya Kiwengwa Kumbaurembo, katika Bonaza la mashairi ya papo kwa papo.
Amesema, Waalimu wa Madrasa wanajitahidi katika kuwafundisha watoto malezi mema kwani muda mwingi wanakuwepo chini ya uangalizi wao hivyo ni vyema kuthamini mchango wanaoutoa bila ya malipo.
Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Hamid Seif Said
“Waalimu wanatumia nguvu nyingi kusimamia vizuri malezi ya watoto wetu, kwani tunapowawezesha na kuthamini michango yao wataongeza ari na kasi ya kufundisha na kuwafanya kuwa watoto wema na bora katika jamii”alisema Mkuu wa Wilaya.
Aidha amesema kuwa wazazi wamekuwa wakitumia gharama kubwa kuwapeleka watoto Skuli na kusahau thamani na mchango wa waalimu wa Madrasa kwa watoto wao jambo ambalo linarejesha nyuma maenedleeo ya walimu hao.
“ Ongezeko la madawa ya kulevya na Udhalilishaji linachangiwa na ukosefu wa malezi bora ya watoto wetu ,ambao unachangiwa na kutokuwathamini walimu wa madrasa hivyo tushirikiane na walimu hao katika malezi ili kuondoa changamoto hizo,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Hamid Seif Said akikabidhi misahafu kwa Walimu wa Madrasa
Aidha amesema, watunzi wa mashairi ni wasanii kama wengine kwani wanaelimisha jamii juu ya mambo mbalimbali, ikiwemo athari za matumizi ya dawa za kulevya, maradhi yasioambukiza na malezi ya watoto.