Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Sauda Mtondoo amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuipatia Wilaya hiyo gari la zimamoto ili kuweza kukabiliana na majanga mbalimbali ya moto yanayoweza kujitokeza.
Kauli ya Mkuu huyo wa Wilaya inakuja baada ya tukio la hivi karibuni ambapo moto uliharibu na kuteketeza sehemu kubwa ya nyaraka za Halmashauri ya Wilaya ya Igunga zilizokuwa zimehifadhiwa katika ghala lililopo Kitongoji cha Kati mjini humo.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Muhoja Masanja amesema chanzo cha moto huo bado hakijafahamiki na kwamba alifika mapema eneo hilo na kuomba msaada kwa wananchi ili kuudhibiti moto huo usisambae zaidi pamoja na kusaidia kuokoa baadhi ya mali na nyaraka.
DC. Mtandoo amesema, “Kwa kweli nimepokea kwa masikitiko kuungua kwa ghala hili la Halmashauri kwani ndani yake kulikuwa na Vitabu na nyaraka mbalimbali zilizohifadhiwa.”
Ameongeza kuwa, katika Wilaya ya Igunga kuna Ofisi ya zimamoto lakini haina vifaa vya kutosha vya uokozi pamoja na uzimaji wa moto, na kuwaomba wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali, katika shughuli za uokozi wa majanga kama hayo.