Mkuu wa Wilaya ya Rorya mkoani Mara, Juma Chikoka maarufu Mchopanga amepokea mbio za Mwenge katika wilaya hiyo ambapo amesema mbio hizo zitatumika kukagua, kutembelea na kuweka mawe ya msingi katika miradi tisa ya Sh2.27 bilioni.

Akizungumza leo Alhamisi Juni 24, 2021 baada ya kupokea mwenge huo  kutoka wilayani Tarime,  Chikoka amesema miradi hiyo ni ya sekta ya afya, maji, elimu, uwekezaji na miundombinu.

Miradi ya  sekta binafsi imepewa kipaumbele kutokana na msisitizo wa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu ushirikiano wa sekta  binafsi na Serikali katika kukuza uchumi wa mtu mmojammoja na Taifa.

“Miradi mingi itakayofikiwa ni pamoja na ya wawekezaji na wajasirimali na hii ni kutokana na umuhimu wao katika kukuza uchumi wa mtu mmojammoja.”

“Kwa kuanzia mwenge utapita katika kiwanda cha mwekezaji mdogo ambaye ameona fursa zilizopo na kufungua kiwanda cha kutengeneza viatu hii ikiwa ni katika kuunga mkono jitihada za Serikali kuwa na Tanzania ya viwanda,” amesema Chikoka.

Naye kiongozi wa mbio hizo za mwenge, Luteni  Josephine Mwambashi amesisitiza kuhusu jamii kujikinga na ugonjwa wa corona na kwamba miongoni mwa ujumbe wa mwenge huo maalum mwaka 2021  ni juu ya tahadhari kuhusu ugonjwa huo.

Zaydi, Niyonzima kuikosa Simba SC Jumamosi
Copa America 2021: Brazil yatangulia Robo Fainali