Mkuu wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Siriel Mchembe na Kamati ya ulinzi na usalama, imemsimamisha kazi mtendaji kata ya Kwenjugo, Athumani Mgaza akidaiwa kutenda makosa 20 ikiwemo kuwafunga pingu wananchi wanaoshindwa kulipa michango mbalimbali.
Kauli hiyo imetolewa na DC Mchembe kwenye mkutano wa kusikiliza kasoro ya ujenzi wa zahanati ya Bwila jana Jumatatu Aprili 18, 2022.
Mchembe ametoa siku saba kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na mkaguzi wa ndani ya Halmashauri kuchunguza tuhuma hizo.
“Mtendaji wa kata ya Kwenjugo anasimama kazi mara moja kupisha uchunguzi wa tuhuma 20 zinazomkabili. Hakuna mtendaji wa kata anayetembea na pingu ili akikosa michango kwa wananchi amfunge, akipishana lugha na mwananchi amtoze Sh20000 “amesema Mchembe
Akizungumza mbele ya wananchi mtendaji wa kata hiyo, Athumani Mgaza amesema alimtoa fundi aliyekuwa anaendelea na ujenzi kwa kukosa vigezo vya kuendelea na kazi hiyo kutokana na kutokuwa na mkataba.
Amesema baada ya tangazo la mkurugenzi kuwataka mafundi wote kuwa na mkataba, walimtaka fundi huyo kuomba mkataba lakini hakufanya hivyo.
“Barua zilizopokelewa mheshimiwa mkuu wa wilaya ni barua nne, huyu mwenzetu kwa sababu alitusaidia tulimbembeleza sana lakini hakufanya hivyo” amesema Mtendaji Athumani.
Katika kikao hicho, Mbunge wa Handeni Mjini, Reuben Kwagilwa amewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa endapo watabaini hujuma kwenye miradi inayoendelea katika maeneo yao.