Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi ameliagiza Jeshi la Polisi kumuweka ndani siku mbili, Afisa Uthamini wa Wilaya hiyo, Einhard Chidaga kwa kosa la kutotekeleza majukumu yake pamoja na kudharau wananchi kitendo kinachodaiwa kusababisha uwepo wa migogoro ya ardhi katika wilaya yake .
Hapi ametoa maagizo hayo leo katika mkutano wake na wananchi wa Kata ya Wazo uliofanyika kwenye viwanja vya Mkanada ambapo ni muendelezo wa ziara yake ya siku kumi.
Hatua hiyo imekuja baada ya wananchi wengi kulalamika kutolipwa fidia zao na manispaa hiyo licha ya uthamini wa viwanja vyao kufanyika, na kwamba ilitakiwa afisa uthamini huyo awepo katika mkutano huo kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa malalamiko ya wananchi lakini hakutokea katika mkutano huku simu yake ya mkononi ikiwa haipatikani.
“Polisi mtafteni huyo mtu, alale ndani masaa 48, anajua kabisa kuwa kuna mkutano wa wananchi na kwamba anahitajika kusikiliza na kujibu malalamiko ya wananchi lakini amezima simu,”amesema Hapi.
Hata hivyo, Hapi amesema kuwa Afisa uthamini huyo hatekelezi majukumu yake inavyotakiwa kwa kuwa tangu ameanza ziara ya kutembelea wananchi ili kujua kero na changamoto zao, Chidaga hajawahi kuhudhuria katika ziara yake ya siku kumi katika wilaya hiyo ya Kinondoni.