Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi ameitaka Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) kusimamia kwa karibu shughuli za ujenzi wa mindombinu ya miradi ya maji katika Wilaya hiyo zinazotekelezwa na kampuni ya ukandarasi ya Wapcos Ltd ya nchini India ili kukamilika kwa wakati kabla ya tarehe 29 Februari mwaka huu.
Akizungumza katika ziara ya kukagua miradi ya ujenzi wa miundombinu ya maji inayosimamiwa na DAWASA katika Wilaya hiyo, Happi alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa Wilaya hiyo inafikia kiwango cha asilimia 95 ya upatikanaji wa maji, hatua inayolenga kuondoausumbufu wa upatikanaji wahuduma hiyo kwa wananchi.
“DAWASA hakikisheni mnasimamia kwa ukamilifu shughuli zote za mkandarasi kwa kuwa hakuna kikwazo cha kumaliza mradi huu katika muda na wakati tuliopanga, pesa zimelipwa na Serikali ipo tayari kutoa kila aina ya ushirikiano unaohitajika katika kukamilisha miundombinu hii ili hatimaye wananchi wetu wapate maji”.
Happi aliutaka Uongozi wa kampuni ya ukandarasi ya Wapcos Ltd, kutambua kuwa utekelezaji wa mradi wa maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni ni mojawapo ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano iliyolenga kukamaliza tatizo la muda mrefu la huduma ya maji katika maeneo mbalimbali ya Manispaa hiyo.
Kwa mujibu wa Happi alisema Serikali ina Imani kubwa na mkandarasi wa kampuni ya ujenzi wa miradi hiyo kuwa atakamilisha kazi hiyo kwa wakati na muda uliopangwa ili kuhakikisha kuwa Serikali za Tanzania na India zinaendelea kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi baina ya Mataifa hayo.
Akifafanua zaidi Happi alisema miradi hiyo, Serikali kupitia DAWASA inajenga tenki kubwa lenye uwezo wa kuhifadhi maji yenye ujazo wa lita Milioni 5, hatua itakayosaidia kumaliza tatizo kubwa la maji linalokabili maeneo yaliyopo katika maeneo ya miinuko ikiwemo Makongo, Changanyikeni pamoja na Goba.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi wa DAWASA, Modesta Mushi alisema kiasi cha Tsh. Bilioni 80 zitatumika katika utekelezaji wa mradi huo ikiwa ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya India.
Mushi alisema lengo la mradi huo ni pamoja na kuhakikisha kuwa wananchi wa kawaida wanapata huduma bora za maji, ambapo katika matanki mapya yatakayojengwa yatasaidia kufikisha maji katika maeneo yote ambayo yamekuwa hayapati maji kutokana na miinuko na kufanya huduma ya maji kuwa bora na yenye uhakika zaidi.
“Maeneo yatakayonufaika na mradi ni pamoja na Salasala, Bunju, Wazo, Makongo, Changanyikeni, Bagamoyo, Mpiji, Zinga, Kiromo, Kitopeni, Ukuni, Bumba pamoja na Mataya” alisema Bi. Mushi.
Naye Meneja Mradi wa Kampuni ya Wapcos Ltd, P.G Rajan aliihakikishia Serikali kuwa kampuni hiyo itafanya kazi hiyo usiku na mchana ili kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati kwa kuzingatia masharti ya mikataba iliyowekwa katika utekelezaji.
“Tulipaswa kukamilisha kazi hii, Mwezi Novemba 2017 lakini kutokana na changamoto kadhaa tulishindwa kufanya hivyo, tunaiahidi Serikali kuwa tutafanya kazi katika muda wote ili kuikamilisha kazi hii kabla ya kufikia muda uliowekwa na Serikali” alisema Rajan.