Mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard Atufigwege Kasesela ameagiza kuwa watoto wote ambao hawajajaza fomu na kuripoti shuleni kwa wakati watafutwe popote walipo na kupelekwa shuleni.
Kasesela ametoa agizo katika ziara ya kushtukiza aliyoifanya katika shule ya Sekondari Tagamenda ya kukagua mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza.
Katika ziara hiyo, Mwalimu mkuu wa shule hiyo ametoa taarifa kuhusu watoto waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza shuleni hapo, ambapo ameeleza kuwa kati ya watoto 180, ni watoto 150 tu ndio waliojaza fomu, na kati yao watoto 125 tayari wameripoti shuleni hapo kuanza masomo na 25 wanatarajiwa kuripoti wakati wowote.
Mkuu wa Shule hiyo amesema hakuwa na taarifa yoyote kuhusiana na watoto 30 ambao mpaka sasa hawajajaza fomu wala kuripoti shule.
Aidha, kuhusu changamoto ya miundo mbinu katika shule hiyo, Kasesela ametoa wito kwa wote waliowahi kusoma shule hiyo miaka ya nyuma na wasamaria wema kujitokeza kuchangia ujenzi wa madarasa kwani madarasa ya kidato cha nne waliomaliza yalikuwa mawili lakini kidato cha kwanza kuna madarasa 6 hivyo kuwepo kwa uhitaji wa kujenga madarasa manne. Pia ilielezwa kuwa shule ya Tagamenda pia inatarajia kuongeza idadi ya wananfunzi wa kidato cha 5.