Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya hiyo, Jokate Mwegelo, ameichukulia hatua kampuni ya Rak Kaolin, ambayo imekuwa ikijihusisha na uchimbaji wa madini ya Kaolin licha ya kuzuiliwa na Naibu Waziri wa Madini Madini Stanslaus Nyongo.

Jokate na Kamati yake walibaini kitendo hicho cha mwekezaji kuendelea kuchimba madini hayo kwenye zoezi la ukaguzi lililofanyika Septemba 06-07 mwaka huu katika maeneo mbalimbali ya shughuli za uchimbaji wilayani humo.

Taarifa ya wilaya hiyo imeeleza kuwa ukaguzi huo ulifanikiwa kukamata malori matatu yenye jumla ya tani 100 za madini hayo.

Serikali ya wilaya ya Kisarawe katika kikao cha pamoja na Kamishna wa Madini Ukanda wa Mashariki Mhandisi Ally Maganga kimeamuru Kampuni hiyo kulipa adhabu ya kukiuka maagizo ya Naibu Waziri, Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya 2017.

Kampuni hiyo ya Rak Kaolin pia imetakiwa kulipa mapato yote ya Serikali ambayo imekwepa huku Jokate akitoa rai kwa wawekezaji wote wilayani humo kuhakikisha wanafuata sheria na kanuni zilizowekwa zikiwemo za kulipa kodi bila shuruti.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Septemba 10, 2018
Obama: huu ni upuuzi