Johansen Buberwa, Kyerwa – Kagera.
Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Zaitun Msofe amekemea vikali tabia ya baadhi ya viongozi wanaoingilia majukumu ya watendaji kuanzia ngazi ya vijiji na kusababisha kushindwa kutimiza majukumu yao kwa ufanisi na wakati.
Msofe ametoa kauli wakati akitoa maelekezo ya serikali katika kikao cha Baraza la Madiwani kwa robo ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 katika Halmashauri ya wilaya ya Kyerwa, ambapo amesema kila mmoja anapaswa kubaki katika misingi ya kazi yake na sio kuingilia majukumu ya mtu yoyote, ili kuepusha migogoro ya kiutendaji.
Amesema, “ni jukumu la watendaji wote kuanzia ngazi ya vijiji kufanya kazi kwa kuzingatia sheria kanuni,taratibu na miongozo iliyopo tusifanye kazi kwa kufuata utashi wetu wala utashi wa mtu mwingine wala Viongozi tuache kuingilia majukumu ya watendaji ambayo yapo kisheria.”
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Wilaya amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kyerwa, James John pamoja na Madiwani kuhakikisha wanatumia wakaguzi wa ndani, ili kupata dondoo mapema na kuzifanyia marekebisho haraka kabla ya ukaguzi wa nje kukuta hoja za kujibu.