Mkuu wa Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, Peter Lijualikali amemuagiza Mkuu wa Polisi Wilaya hiyo kumkamata na kumhoji Kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA, Godbless Lema kwa tuhuma za kutoa kauli ya kuhatarisha maisha ya Mtendaji wa Kijiji cha Korongwe Forodhani.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma, .Lijualikali amesema kauli hizo zilizotolewa na Kiongozi huyo zimesadifu hoja ambazo zimekuwa zikielekezwa kwao kuwa, Chama hicho kinafuga vikundi vya kufanya vitendo vya kiuhalifu.
Amesema, “OCD wa Nkasi namuagiza kuchukua hatua za kisheria mara moja, kufanya upelelezi dhidi ya uchochezi wa mauaji aliofanya Lema na kuhatarisha uhai na maisha ya watu na hali ya usalama katika eneo letu, hali ambayo inakwaza juhudi za wananchi katika kujishughulisha na shughuli za maendeleo.”
Lijualikali amedai Oktoba 24, 2023, Lema akiwa kijijini hapo kwenye mkutano wa hadhara alitoa kauli yenye ukakasi inayosababisha ofisa huyo kuishi kwa hofu baada ya kusikika na kuonekana akitoa kauli za kuchochea mauaji kwa kuhamasisha vikundi vya chama hicho kuchaukua hatua kinyume na sheria.