Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Victoria Mwanziva amezindua Kituo cha Afya Mundindi kilichogharimu kiasi cha zaidi ya sh. Mil. 500 ambapo uzinduzi wa kituo hicho uliambatana na mapokezi ya vifaa tiba vyenye thamani ya sh. Mil. 150.

Kwa mujibu wa taarifa ya ujenzi wa kituo hicho iliyowasilishwa kwa mkuu huyo wa wilaya katika hafla ya uzinduzi huo imeeleza kuwa kituo hicho cha afya kinaenda kunufaisha wakazi zaidi ya elfu arobaini wa Tarafa ya Liganga ambao hapo awali walikuwa wakikumbwa na changamoto juu ya upatikanaji wa huduma hiyo.

Akizindua kituo hicho, Mkuu huyo wa Wilaya amesema Wilaya ya Ludewa imepokea fedha za kuboresha huduma ikiwemo sh. Mil 900 za kuboresha miundombinu ya majengo ya Hospitali ya Wilaya hiyo, Mil. 200 za kukamilisha Zahanati ya Kitongoji cha Chimbo na Zahanati ya Mkiu Kimelembe ambazo zimekamilika na kuanza kutoa huduma, hukuZahanati ya kijiji cha Ndowa ujenzi wake ukiendelea.

Kuhusu mapokezi ya vifaa tiba, Mwanziva amewaagiza watoa huduma kuvitunza vifaa hivyo ili viweze kutumika kwa muda mrefu, huku akiyaomba mashirika na wadau wa afya kuendelea kuunga mkono uboreshaji wa huduma za afya kwa kuleta vifaa tiba ili wananchi waweze kupata huduma iliyo bora zaidi.

Amesema, “tunamshukuru mama yetu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na mbunge wa jimbo la Ludewa kwa ushiririkiano wao uliowezesha kupatikana kwa fedha hizo za miradi kwani Rais huyo amekuwa akifika kusiko fikika kwa kuleta Fedha za kuboresha miundombinu hii ya afya na si hizo tuu bali hata katika miradi mingine kama ya elimu na barabara.”

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya pia amezindua Zahanati ya Kitongoji cha Chimbo ambayo imegharimu kiasi cha zaidi ya Sh. Mil. 74 na miongoni mwa fedha hizo Mil. 50 imetolewa na serikali na nyinginezo ni michango ya wananchi na wadau mbalimbali wa afya.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Sunday Deogratius amesema amewapongeza wananchi kwa kujitoa kuanzisha ujenzi miradi mbalimbali ya maendeleo zikiwemo zahanati na vituo vya afya ambapo amewataka kuendeleza jitihada hizo za kujitoa katika maendeleo ambapo serikali itawaunga mkono badala ya kukaa na kusubiri serikali ianzishe miradi hiyo.

Amesema, “Ndugu zangu ujio wa fedha hizi za maendeleo, upatikanaji wa vifaa tiba na fedha za umaliziaji miradi ya ujenzi zinakuja kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na Mbunge wetu Joseph Kamonga ambaye tumekuwa tukifanya nae kazi bega kwa bega na amekuwa akizunguka katika Wizara mbalimbali ili kuona namna ya kupata fedha za maendeleo ya jimbo.”

Watanzania wanataka Umeme wa uhakika - Dkt. Biteko
Baadhi ya Wanafunzi hawajafanya Mtihani Darasa la saba