Boniface Gideon – TANGA.

Msimu mpya wa Maonesho ya Biashara yanayohusisha Wajasiriamali wanawake mkoani Tanga, maarufu Tanga Women Gala umezinduliwa rasmi na yanatarajia kuwakutanisha Wafanyabiashara na Wajasiriamali hao zaidi ya 200 kutoka mikoa yote nchini.

Akizindua maonesho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa amewataka Wajasiriamali wayatumie kama sehemu ya kutangaza Biashara zao na si kufikiria uuzaji wa Biashara pekee.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Five Brothers Entanglement Nasoro Makau (katikati), akikata keki kuashiria kuanza kwa msimu mpya wa Maonesho ya Biashara ya Tanga women gala msimu wa 6 yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Sept 27 – 30, 2023 Jijini Tanga.

Amesema, “miongoni mwenu mkifika kwenye maonesho mnafikiria kuuza mzigo mlionao kwa siku hizo za maonesho, mkimaliza mnasema faida mmepata mwisho wa siku mnaendelea na maisha mengine, badilikeni na mtumie jukwaa hili kutafuta masoko muda wote kwa kujikita kutangaza Biashara zenu na sio kuuza tu wakati wa maoyesho.”

“Nawapongeza kwa mchango wenu kwa jamii ya wana Tanga, Serikali yetu imetengeneza fursa nyingi ikiwemo kutoa wigo kwa wajasiriamali na wafanyabiashara kufanya biashara zao vizuri bila changamoto zozote niliona kama kiongozi wa wilaya niwapongeze na niwatake muendeee kufanya hivyo hivyo siku zote,” alisema Mkuu huyo wa Wilaya, Hashim Mgandilwa.

)Baadhi ya Wajasiriamali watakaoshiriki Maonesho ya Biashara ya Tanga women gala msimu wa 6 wakisiliza ratiba za maonesho hayo Jana Wakati wa uzinduzi wa Maonesho hayo Jijini Tanga.

Awali, Mkurugenzi wa Kampuni waandaaji ya Five Brothers Entertainment, Nasoro Makau alisema maonesho hayo yameingia msimu wa sita na yatafanyika rasmi Septemba 27 – 30, 2023 huku wakiwa na matumaini kuwa yanakwenda kutengeneza historia kubwa ambayo itakuwa chachu ya kuendelea kuwainua wajasiriamali na kukua kiuchumi.

“Tanga Women Gala ni Jukwaa la Wajasiriamali ambalo limekuwa likifanyika kila mwaka kwa lengo la kuhakikisha wanakua na kuinuka kiuchumi kwa kupanua wigo wa kibiashara na msimu huu wa sita wa Tanga Women Gala Wajasiriamali watakwenda kufanya mambo makubwa.” aliongeza Makau.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Juni 26, 2023
Nape: Gharama ya mawasiliano haijapanda