Wachimbaji wanne wamefukiwa na kifusi katika machimbo ya kokoto yaliyopo Pugu jijini Dar es salaam huku mmoja akiokolewa akiwa hai na wengine watatu wakiwa tayari wameshafariki.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya Ilala, Sophia Mjema mara baada ya kushiriki zoezi la uokoaji katika machimbo hayo, amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kwa wananchi kuendelea na shughuli za uchimbaji katika eneo hilo kwani lilishazuiliwa.
Amesema kuwa Sheria kali zitachukuliwa kwa mtu yeyote atakaye endelea kuchimba kokoto katika machimbo hayo kwani ni hatari na eneo hilo lilishapigwa marufuku kuendesha shughuli hizo.
“Sisi kama Serikali tumeliona hili ni hatari sana, nina agiza tena kwa mara nyingine hakuna mtu yeyote kuchimba kokoto hapa, na ni lazima tuwatafute watu wote walio shiriki kutoa kibali cha uchimbaji katika eneo hili,”amesema Mjema.
Aidha, amesema kuwa ajira ya machimbo hayo imefungwa na hairusiwi tena kufanya shughuli za uchimbaji, hivyo amewashauri wananchi kubuni ajira kama za kilimo na biashara lakini si za machimbo hayo.
Vile vile amewaomba Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kushirikiana kwa umoja ili kuweza kuwabaini wale wote waliokuwa wamejimilikisha maeneo ya uchimbaji katika eneo hilo la pugu.
Hata hivyo, Mjema amewaasa wananchi kuwa wasikivu pindi linapotolewa zuio la uchimbaji katika maeneo ambayo ni hatarishi kama hayo kwani yanaweza kusababisha maafa makubwa pasipo na sababu zozote za msingi.