Scolastica Msewa – Pwani.

Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Nasri Ally amepiga malufuku kuongeza kiasi chochote cha fedha kwenye Viuatilifu aina ya Salfa vya zao la Korosho, vilivyosambazwa na Serikali Wilayani humo na Serikali kwa Wakulima.

Khadija ameyasema hayo mjini Mkuranga, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa Wajumbe wa Halmashauri kuu ya Chama hicho Wilaya akidai Viuatilifu hivyo hutolewa bure kwani ni ruzuku kutoka Serikalini vikilenga kumsaidia mkulima wa Korosho ili anufaike na kilimo.

Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Nasri Ally.

Amesema, “hatutaki Mheshimiwa Rais agombanishwe na Wananchi wa Wilaya ya Mkuranga alitafuta fedha na akahakikisha Salfa inakuja bure, kwahiyo naomba tukayasimamie hayo katika Kata zetu na mkawaeleze Wakulima Salfa ni haki yao kuipata bila kutoa hata senti moja, hayo ndio maelekezo kutoka kwa Mheshimiwa Rais.”

Akizungumza kwa Njia ya simu Mwenyekiti wa Chama kikuu cha Ushirika wa Wakulima mkoa wa Pwani – CORECU, Musa Mng’eresa amesema kulikuwa na vyama vya msingi – AMCOS vitatu vya Kata ya Magawa Wilayani Mkuranga ambavyo viliwatoza gharama za usafiri Wakulima wakati wa kuchukua Salfa zao, lakini baada kupewa maelekezo waliacha.

Mwenyekiti wa Chama kikuu cha Ushirika wa Wakulima mkoa wa Pwani – CORECU, Musa Mng’eresa.

“Sisi CORECU kama Ushirika tulipeleka Salfa hizo hadi kwenye vyama vyote vya msingi mkoani Pwani lakini wale Viongozi wa vyama walikuwa wanafanya huo ubadhirifu kwa kuwaambia Wakulima wachangie kwa mfuko Kati ya shilingi 1,000 hadi 1,500 nasisitiza hizo dawa zimekuja za bure zimetolewa na serikali,” alisema Mng’eresa.

Aidha aliongeza kuwa, “na sisi CORECU tumewasambazia Wananchi kama inavyotakiwa kwahiyo ni malufuku Chama chochote cha msingi kumchaji mkulima yeyote kiasi chochote kuhusu hiyo Pembejeo, na anayechukua hizo pembejeo awe na shamba tutakuja kuhoji Salfa ulizochukua umepeleka wapi asipoonesha alikopeleka hatua kali za kisheria zikichukuliwa dhidi yake.”

Ngoma, Mzamiru wampasua kichwa Robertinho
Zimamoto watoa darasa kwa Wanafunzi Pwani