Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri, ameyataka makampuni
yanayojishughulisha na biashara ya mafuta na gesi kuimarisha mifumo ya kulinda afya na usalama wa wafanyakazi ili kuepuka athari zinazoweza kutokea endapo hakutakuwa na mifumo hiyo.
Ameyasema hayo alipofungua kikao cha mashauriano baina ya wadau wa sekta ya mafuta na gesi na menejimenti ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kilichofanyika katika ofisi ya Mkuu huyo Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kuhitimisha kikao hicho, Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema madhumuni ya kikao ni kujenga uelewa wa pamoja kuhusu sheria na kanuni mbali mbali kuhusu afya na usalama kazini miongoni wadau wa sekta ya mafuta na gesi.
Baadhi ya washiriki wa kikao wameishukuru serikali kupitia OSHA kwa kuandaa kikao hicho ambapo wamesema imekuwa ni fursa muhimu kwa pande zote mbili (OSHA na wadau) kujadiliana masuala ya msingi ambayo yatasaidia kuboresha mifumo ya usalama na afya katika sekta ya mafuta na gesi ambayo shughuli zake ni hatarishi zaidi kiusalama na afya.
OSHA ni taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu ambayo in jukumu la kusimamia Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake ambazo zina lengo la kuwalinda wafanyakazi dhidi ya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.