Viongozi watano wa Serikali ya kijiji cha Isuki, wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wametiwa mbaroni kwa tuhuma za ukatili dhidi ya wanawake ambao huwakamata na kuwacharaza viboko 60, kuwatoza fedha, na kuwapaka upupu sehemu za siri.
Kutokana na vitendo hivyo vya kukamatwa, kufungiwa na kuteswa katika mahabusu ndogo ya kijiji hicho iitwayo Goligotha, Mkuu wa Wilaya hiyo, Lengai Ole Sabaya ametangaza kufuta utaratibu wa sungusungu kufanya operesheni ndani ya kijiji hicho.
Pia ameamuru kukamatwa na kuhojiwa na TAKUKURU, viongozi hao ambao ni Mwenyekiti wa serikali ya kijiji Rabikira Makere, Mjumbe wa Serikali ya kijiji, Tekla Assenga na wenyeviti watatu wa vitongoji.
Mmoja wa waathirika Neema Ng’unda ameliambia gazeti la Nipashe kuwa baada ya kukamatwa majira ya saa 1: 15 usiku, alifungwa pingu na kupelekwa katika jengo la Goligotha na kupakwa washawasha baada ya kushindwa kulipa faini ya sh. 30,000.
DC Sabaya amesema kuwa ” Hakuna mtu yeyote mwenye mamlaka ya kuwashurutisha wananchi walale saa 2:00 usiku, isipokuwa Rais John Magufuli. Ni kinyume cha utaratibu na sheria na ni ukanyagaji wa katiba ya nchi”
Vivyo hivyo ameagiza fedha zilizokuwa zikitozwa kutokana na ukatili huo zirudishwe kwa wananchi na kituo kidogo cha polisi Losaa ambacho kilifungwa, kifunguliwe na kutoa huduma kwa wananchi wakijiji hicho na vijiji jirani.