Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya – DCEA, imesema imejipanga kuhakikisha inapambana na kutokomeza Dawa za kulevya, kwa kufanya operesheni mbalimbali nchi nzima na kutoa elimu juu ya madhara ya dawa hizo, ili Taifa liweze kuwa na uchumi na nguvu kazi imara.
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya – DCEA, Aretas Lyimo ameyasema hayo wakati akiongea na Dar24 Media jijini Dar es Salaam kuhusu zoezi la utoaji wa elimu kwa jamii juu ya sheria zinazoongoza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, madhara na aina ya Dawa za kulevya.
Amesema, “tumeandaa muongozo wa ufundishaji ambao kupitia NGO’s, wadau wetu mbalimbali na Wizara ya Elimu Wanafunzi na jamii watakuwa na uelewa wa Dawa za kulevya na jinsi ya kuepukana nazo na madhara yake, na kuna mchakato unaendelea ili kuingiza somo la Dawa za kulevya kwenye mitaala.”
Kamishna Jenerali Lyimo ameongeza kuwa, somo hilo litakuwa likifundishwa kuanzia ngazi ya msingi mpaka vyuo na linalenga kuepusha kundi kubwa la Vijana kutokujiingiza kwenye matumizi ya Dawa za kulevya.