Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka nchini England Pep Guardiola amesema Kiungo wa kati kutoka Ubelgiji Kevin De Bruyne anaweza kukosekana kwa kipindi cha miezi minne ijayo huku klabu hiyo ikipanga kuamua iwapo mchezaji huyo anahitaji kufanyiwa upasuaji wa jeraha la misuli ya paja.
De Bruyne alichechemnea katika kipindi cha kwanza cha ushindi wa 3-0 wa City dhidi ya Burnley ljumaa (Agosti 11) baada ya kujirudia kwa tatizo hilo ambalo lilikatiza ushiriki wake katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Juni.
Akizungumza kabla ya mchezo wa Super Cup uliopigwa jana Jumatano (Agosti 16) dhidi ya Sevilla CF mjini Athens, Guardiola aliwaambia waandishi wa habari: “Ni jeraha baya. Tunapaswa kufahamu ama anahitaji upasuaji au hakuna upasuaji lakini atakuwa nje kwa miezi michache. Uamuzi wa upasuaji utachukuliwa katika siku chache zijazo. Itakuwa kati ya miezi mitatu au minne,”
De Bruyne alikosa mechi za City kabla ya msimu mpya lakini akarejea katika kipindi cha pili cha kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii walipofungwa na Arsenal.