Baada ya kuambulia sare ya pili mfululizo katika Ligi Kuu ya England dhidi ya Southampton, Mlinda Lango wa Man Utd David De Gea amesema huenda mambo yanawaendea kombo kutokana na Imani za Kishirikina.
Man utd iliambulia sare ya 1-1, Licha ya kutangulia kwa bao la kiungo Mshambuliaji Jadon Sancho dakika ya 21, huku bao la Southampton likifungwa na Che Adams dakika ya 48.
Mlinda Lango huyo kutoka nchini Hispania amesema huenda Laana na Imani za Kishirikina zinawapa wakati mgumu kupata matokeo kama wanavyotarajia, kwani haamini kinachoendelea kutokea klabuni hapo.
“Ninadhani mtu alituroga. Ukweli ni kwamba sielewe kinachoendelea, sielewi kabisa,” amesema De Gea katika mahojiano na gazeti moja la Uhispania la El Pais.
Ndoto ya Man United kuokoa msimu wao huenda isitimie klabu hiyo sasa ikipeleka nguvu zake kujihakikishia nafasi ya nne bora katika Ligi Kuu ya Uingereza, lakini hilo pia kwa sasa linaonekana kuwa mtihani mgumu.
Klabu hiyo ilianza msimu ikiwa na matumaini ya kupigania taji la EPL, lakini imedhihirika wazi kuwa United huenda wakamaliza msimu mwingine bila kushinda taji lolote.
Man Utd imekuwa katika wakati mgumu tangu Meneja wao Mashuhuri Sir Alex Ferguson alipostaafu mwaka 2013 na mara ya mwisho kushinda taji lolote ni mwaka 2017.
Klabu hiyo ilitarajiwa kupigania taji la EPL msimu huu lakini sasa hata kumaliza katika tano la nne bora inaonekana kuwa mtihani mgumu.