Miamba ya soka mjini Madrid, Hispania Real Madrid inafikiria kumchukua kocha wa Brighton, Roberto De Zerbi ili akachukue mikoba ya mkongwe Carlo Ancelotti.
Awamu yake ya pili ya ukocha huko Bernabeu, Ancelotti itafika kikomo 2024, hiyo ina maana ni mwisho wa msimu huu.
Ancelotti yupo kwenye kikosi cha Los Blancos kwa muda sasa, ambapo msimu uliopita alifanikiwa kuwapa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini hana muda atapeana kisogo na miamba hiyo.
Na sasa mabosi wa Bernabeu wanakuna kichwa kupata mtu wa kuja kuchukua mikoba yake na hapo wanampiga De Zerbi kwa mujibu wa Cadena SER.
De Zerbi yupo Brighton kwa mwaka mmoja tu baada ya kuchukua mikoba ya Graham Potter na msimu uliopita aliwasaidia kushika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
De Zerbi amepata sifa kubwa kutokana na staili ya soka lake huku uwezo wake ukipongezwa na makocha hodari kama Pep Guardiola.
Katika msimu huu wa Ligi Kuu England, Brighton imeshinda mechi tano kati ya sita huku kocha De Zerbi mwenye umri wa miaka 44, akiendelea kuonyesha ufundi wake katika kuandaa timu makini ndani ya uwanja.
Ukimweka kando De Zerbi, mtu mwingine anayepigiwa hesabu na Real Madrid ni kocha wa Bayer Leverkusen, Xabi Alonso, ambaye aliwahi kuichezea klabu hiyo ya Bernabeu. Alonso alianzia kazi yake ya ukocha huko Real Sociedad.
Wakati akiwa mchezaji, Alonso alizichezea pia Liverpool na Bayern Munich na huko alipata nafasi ya kuwa chini ya makocha mahiri kama Rafa Benitez, Pep Guardiola na Ancelotti, ambaye atakuwa Kocha wa timu ya taifa ya Brazil atakapoondoka Real Madrid.