Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amefichua kuwa atakuwa tayari kumchezesha Declan Rice nafasi ya beki kama ikitokea dharura.
Rice anayecheza nafasi ya kiungo amekuwa moja ya usajili bora wa Arsenal baada ya kununuliwa kwa Pauni l05 milioni kutoka West Ham, sasa anajiandaa kupewa majukumu mapya.
Kiungo huyo amekuwa na mchango mkubwa kwenye dimba la kati katika mbio za kuwania ubingwa msimu huu 2023/24, pamoja na Ligi Mabingwa Barani Ulaya baada ya kufuzu raundi ya 16 bora.
Baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na PSV juzi Jumanne (Desemba 12) usiku, kwenye mechi ya mwisho ya hatua ya makundi, Arteta amemsifu Rice na kuweka wazi mipango yake kwa ajili ya kiungo huyo.
Tuna uhaba wa mabeki, nataka nijaribu kama jambo likitokea, nawezaje kutatua, nadhani alicheza vizuri dhidi ya PSV, aliwahi kucheza nafasi ya beki.
Tunatakiwa kujaribu kama ikitokea dharura, kwanza tuwe na uhakika kama ataweza kuziba hilo pengo, ni mtulivu sana anapokuwa na mpira, anakaba vizuri,” alisema Arteta.
Rice alicheza nafasi ya beki dhidi ya PSV akitokea benchi akichukua nafasi ya William Saliba akiisaidia Arsenal kumaliza kileleni kwenye kundi lao.
Arsenal bado imeendelea kuwakosa Jurrien Timber na Takehiro Tomiyasu kutokana na majeraha huku Arteta akiwapanga Ben White na Jakub Kiwior upande wa pembeni.
Hata hivyo, matumaini ya Arsenal ya kubeba ubingwa msimu huu yameanza kuingia dosari baada ya kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Aston Villa.
Baada ya kichapo hicho Arsenal imeshuka hadi nafasi ya pili ikiwa na pointi 36 tofauti ya pointi moja na Liverpool iliyoko kileleni kwa pointi 37.