Kiungo kutoka England Declan Rice huenda akabadilishiwa nafasi yake ya kucheza ndani ya uwanja na Kocha Mikel Arteta wakati atakapokamilisha uhamisho wake wa kujiunga na Arsenal.
Staa huyo atakayetua Emirates kwa ada ya Pauni 105 milioni anapewa nafasi kubwa ya kwenda kuipa nguvu kubwa Arsenal katika mbio za kunasa ubingwa wa Ligi Kuu England.
Na sasa, Rice yupo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wake wa kujiunga na Arsenal baada ya kufikiwa kwa makubaliano na klabu yake ya West Ham United.
Makubaliano juu ya ada hiyo itakavyolipwa ilifikiwa Alhamisi iliyopita na Rice alipewa ruhusa ya kwenda kupima afya huko Arsenal baada ya kukubaliana pia maslahi binafsi.
Kutokana na Granit Xhaka kupiga hesabu za kuondoka, Rice anatajwa ndiye atakayekwenda kuchukua mikoba yake na hivyo anaweza kwenda kucheza nafasi tofauti kabisa.
Alipokuwa West Ham, Rice alikuwa akicheza kwenye kiungo cha wachezaji wawili, akisimama mbele ya mabeki wa kati lakini huko Arsenal, atakwenda kucheza upande wa kushoto kwenye safu ya viungo watatu, nafasi ambayo alikuwa akicheza Xhaka.
Majukumu hayo mapya yatamshuhudia Rice, 24, akienda kucheza Namba 8 badala ya Namba 6, mahali ambako alitumika kwenye sehemu kubwa ya maisha yake ya soka. Rice anatazamiwa kushiriki zaidi kushambulia akitokea nyuma.
Arsenal imepania kuwa tishio kwenye Ligi Kuu England msimu ujao ikiwa ishamnasa tayari Kai Havertz kutoka Chelsea na imefikia makubaliano ya kumsajili beki wa Kidachi Jurrien Timber kutoka Ajax.