Mkurugenzi wa Michezo wa FC Barcelona, Deco, amesema Xavi Hernandez anabakia kuwa kocha bora wa klabu hiyo licha ya kushuka kwa kiwango cha timu hivi karibuni.
Xavi aliiongoza Barca kutwaa taji la Ligi Kuu Hispania, La Liga, msimu uliopita ambayo ilikuwa kampeni yake ya kwanza kamili kuinoa klabu hiyo baada ya kuchukua mikoba mwaka 2021 lakini matokeo ya mwaka huu yameongeza shinikizo kwenye nafasi yake.
Barca tayari wamepoteza pointi dhidi ya Getafe, Mallorca na Granada kwenye ligi, huku vipigo viwili katika mechi zao nne zilizopita, dhidi ya Real Madrid na Shakhtar Donetsk, vilisababisha ukosoaji mkubwa kwenye vyombo vya habari.
Timu hiyo ya Katalunya iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Alaves Jumapili (Novemba 12), lakini kama ilivyokuwa kwa Real Sociedad wiki moja kabla, licha ya kushinda mechi hiyo.
Xavi alikiri uchezaji ulikuwa wa kiwango cha chini kwa kile kinachotarajiwa klabuni hapo.
“Sina shaka kwamba Xavi ndiye kocha bora wa Barca, alisema Deco akiiambia Diario Sport.
“Alikubali changamoto ya kuchukua nafasi katika wakati mgumu na yeye ndiye kocha kamili wa kutekeleza ujenzi tunaoendelea nao.”
Xavi alichukua mikoba ya Ronald Koeman miaka miwili iliyopita akiwa na Barca nafasi ya tisa kwenye LaLiga na baada ya kupanda kwenye msimamo na kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya msimu wa 2021-22, aliwaongoza ‘Blaugrana’ hao kutwaa taji lao la kwanza la ligi katika miaka minne msimu uliopita.