Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli leo, Septemba 17, 2019 ametengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya (DC) ya Malinyi Mkoani Morogoro, Majura Mateko na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri (DED) ya Malinyi, Mussa Mnyeti.
Hayo yamejiri baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana, Septemba 16, 2019 kueleza kuwa amechukizwa na mgongano uliopo baina ya viongozi hao na kutoa agizo kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora kwenda kuchunguza weledi wa utendaji kazi wao.
Waziri Mkuu alitoa maelekezo hayo wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Malinyi pamoja na wananchi katika makutano wa hadhara, akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.
Alisema Serikali imewapa nafasi hiyo ili wakasimamie maendeleo ya wananchi na inapeleka fedha kwaajili ya kuboresha maendeleo ya jamii kama kuimarisha huduma za afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara lakini wao wanagombania miradi na mingine wanaichakachua.
Awali Mbunge wa jimbo la Malinyi Dkt. Haji Mponda alimweleza Waziri Mkuu kuwa kwenye Wilaya hiyo kuna matatizo ya mahusiano kati ya Serikali na halmashauri jambo linalosababisha kukwama kwa shughuli za maendeleo.
Ikumbukwe kuwa Rais Magufuli amekuwa akitoa onyo mara kadhaa juu ya migogoro iliyopo kwa baadhi ya wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wakuu wa mikoa.