Mshambuliaji kutoka nchini Serbia Dejan Georgijevic amesema katika muda mfupi tangu alipotua nchini baada ya kusajiliwa Simba SC, amefahamu ukubwa wa klabu hiyo na atahakikisha anawapa furaha Mashabiki na Wanachama kila atakapopata nafasi ya kucheza.

Mshambuliaji huyo amekua gumzo tangu alipojiunga Simba SC, na wadau wengi wa Soka la Bongo wameibua mjadala wa kuhoji uwezo wake, huku wengi wakisema ana uwezo na wengine wakimbeza.

Tayari Dejan ameshapata nafasi ya kuitumikia Simba SC katika Michezo miwili ya Simba, dhidi ya St George ya Ethiopia (Tamasha la SIMBA DAY) na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Young Africans.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Mshambuliaji huyo Dejan ameandika: “Licha ya kwamba nimekuwa sehemu ya Familia ya Simba kwa siku chache tu, nashiriki uchungu na mfadhaiko wa kupoteza mechi yetu dhidi ya wapinzani wetu”

“Ninajihesabu kama mpambanaji asiyekubali kushindwa kama mtu wa nchi yangu, Novak Djokovic. Kwa heshima niliyo nayo kwa mamilioni ya wanasimba, nitateseka, nitajitahidi, nitajitolea na kufanya lolote liwezekanalo ili kutoa huduma bora kwa timu yangu.

“Nitafunga mabao na kuwafurahisha mashabiki, kujivunia na kuwa upande wa ushindi kila wakati” ameandika Dejan kwenye ukurasa wake wa Instagram

Ulimboka Mwakingwe: Mzungu atawashangaza wengi
Ahmed Ally: Kuna watu wamedhamiria kuichafua Simba SC