Chama cha Democratic kimefungua rasmi shauri mahakamani wakiishtaki Urusi, timu ya kampeni ya rais Donald Trump na tovuti ya wikileaks kwa tuhuma za kushirikiana kuchakachua uchaguzi wa urais wa mwaka 2016.
Kwa mujibu wa nyaraka za kesi hiyo, zinadai Trump na timu yake walikubali mpango uliowasilishwa kwao na Urusi ukiwa na lengo la kuwasaidia kuhakikisha wanashinda uchaguzi huo.
Trump na timu yake wamekuwa wakipinga vikali tuhuma hizo dhidi yao wakieleza kuwa zimepikwa kwa lengo la kuwachafua.
Shirika la upelelezi la Marekani katika uchunguzi wake lilieleza kuwa Urusi ilishiriki kujaribu kufanya udukuzi kwenye uchaguzi huo kwa lengo la kumsaidia Trump.
Kesi hiyo imefunguliwa katika mahakama ya Manhattan ikiwahusisha maafisa waandamizi wa kambi ya Trump ikiwa ni pamoja na mkwewe Kushner na Mwenyekiti wa Kampeni, Paul Manafort. Muasisi wa tovuti ya Wikileaks , Julian Assange pia ameunganishwa katika kesi hiyo.
Aidha, wachambuzi wa siasa za Marekani wanaeleza kuwa kesi hiyo inaonekana kama yenye lengo la kuongezea umaarufu chama hicho kwani hata kama Mahakama itaruhusu iendelee, hakuna kitu kipya kitakachoibuliwa tofauti na kile kilichoripotiwa na CIA.