Kiungo kutoka DR Congo na Klabu ya Mtibwa Sugar Deo Kanda amesema imekua bahati mbaya kwao kupoteza dhidi ya Simba SC kwa idadi kubwa ya mabao, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzana Bara.

Mtibwa Sugar jana Jumapili (Oktoba 30) ilipoteza kwa kufungwa 5-0 dhidi ya wenyeji wao Simba SC katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku wachezaji Pascal Kitenge na Casian Ponela wakionyeshwa kadi nyekundu.

Kanda ambaye aliwahi kuitumikia Simba SC kwa mkopo akitokea TP Mazembe msimu wa 2019-20, amesema matokeo yaliyowafika ni sehemu ya mpira, na anaamini wenyeji wao walitumia uzoefu kuwashinda ndani ya dakika 90.

Amesema Simba SC ni timu kubwa ilifahamu wapi ingewazidi kimchezo, na ndicho kilichotokea hadi kukubalia kufungwa 5-0.

“Unajua Simba SC ni timu kubwa, imetumia uzoefu kutushinda ndani ya dakika 90, tumekubaliana na hali hii ya kupoteza na tunakwenda kujiandaa kwa mchezo ujao,”

“Maamuzi ya kadi nyekundu nisingependa kuyatolea ufafanuazi kwa sababu yanabaki kwa mwamuzi mwenyewe, lakini jambo kubwa hapa ni kwamba tumepoteza mchezo, hatuna budi kukubaliana na hilo.” amesema Deo Kanda

Kupoteza kwenye mchezo dhidi ya Simba SC, kumeifanya Mtibwa Sugar kusalia na alama 15 zinazoiweka kwenye nafasi ya nne, sawa na Namungo FC inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na alama 15.

Kero ya Maji: Serikali yashauriwa kukaa na wadau
Kitenge: Ninajutia kosa langu, nimeigharimu timu