Licha ya Uwepo wa malalamiko ya Madereva kuwa Vifaa vilivyotengenezwa maalumu kwa ajili ya kusoma mwendokasi wa Magari vinakinzana na uhalisia pindi wanapokamatwa, Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limesema Vifaa hivyo ni vya Kisasa na vinafanya kazi vizuri.
Hayo yamebainishwa na wakati akitoa elimu ya jinsi kifaa hicho kinavyofanya kazi mbele ya Kamera za Dar24 Media na kuongeza kuwa kwa wale wenye ukakasi juu ya suala hilo wanaweza kujitokeza kwa wataalamu wa Jeshi hilo ili waweze kupatiwa elimu sahihi badala ya kuendelea kulalamika kwa hoja siziso na mashiko.
Amesema, “vifaa hivi ni vya kisasa havina shida yoyote wala ukinzani wa kusoma mwendokasi wa gari, watu wanalalamika lakini kwa hoja ambazo si sahihi, waje tuwaelimishe ili wawe na uelewa juu ya vifaa hivi kwasababu kifaa hiki kinaposoma kitaonesha muda, siku kwa maana ya tarehe na picha sahihi ya tukio na kama haitaonesha hivyo basi upigaji haukuwa sawa.”
Hata hivyo, amesema ni haki ya Dereva kujua ni kiasi gani cha mwendokasi aliokamatwa nao wakati kifaa hicho kikirekodi kumbukumbu huku akitoa rai kwa Askari wa Barabarani kuwa wepesi kutoa maelezo kwa usahihi Wananchi pale wanapohitaji kupata ufahamu ili waweze kuelewa kwa ufasaha tukio husika na kupunguza malalamiko.