Kamanda wa Polisi Mkoani Lindi, Pili Mande amesema chanzo cha ajali iliyouwa watu saba na wengine 22 kujeruhiwa ilisababishwa na Basi la Saibaba kutaka kulipita Gari kubwa la mizigo lililokuwa mbele yake kitendo kilichopelekea kugongana uso kwa uso na Basi dogo la abiria Kampuni ya Baharia.
Ajali hiyo, ilitokea eneo la Kiwawa lililopo Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, ikihusisha basi la hilo kampuni ya Saibaba linalofanya safari zake kati ya Nachingwea na Dar es salaam na Basi dogo la Baharia linalofanya safari zake Dar es Salaam kwenda Wilayani Tandahimba, Mtwara.
Amesema, “baada ya kutokea kwa ajali hiyo mbali na vifo kuna majeruhi watatu ambao hali zao ni mbaya na majina yao bado hayajafahamika na kati yao Wanawake ni wawili na mtoto mdogo wa kiume ambao wote wanahudumiwa katika Hospitali ya Kinyonga iliyopo Wilayani Kilwa.”
Aidha, Kamanda Pili pia amewataja waliofariki Dunia kuwa ni Dereva wa Basi la Saibaba ambaye ni mkazi wa Arusha, Lucas John (59), aliyefariki papohapo na Dereva wa Basi dogo la Baharia, Dereva wa gari ndogo ya Baharia, Omari Ally Abdalah (49), huku miili ya Watu wengine watano ikiwa bado haijatambuliwa.