Mwenyekiti wa kamati ya matibabu ya Shirikisho la soka duniani FIFA, Michel D’Hooghe, anaamini kuwa ligi kuu zote duniani zitafutwa na kuanza upya mwezi August mpaka September kwa sababu ya ugonjwa wa Corona.
Akizungumza kupitia mtandao wa The Daily Telegraph, MWenyekiti huyo amesema kuwa mpira umekuwa mchezo muhimu sana kwenye dunia ya sasa lakini anapendekeza ligi zote zifutwe kwa sababu ya kuepusha ugonjwa huo ndani ya uwanja na nje ya uwanja .
“Nitakuwa na furaha kama ligi zote duniani zitafutwa na ligi hizo zijiandae msimu ujao wa mwaka 2020-2021 kila nchi inahitaji iwe makini na ugonjwa huu kwa sababu watu wengi wamekuwa wanakufa kila siku.
“Kwa sasa pia nchi nyingi zimeyumba kiuchumi kwa sababu ya watu hawafanyi kazi na baadhi ya nchi wamekuwa wakitoa misaada kwenye zilizoathirika na ugonjwa huo wa dunia nina hofia wachezaji wengi wamekuwa wanapenda sana kutema mate uwanjani hii inaweza kupelekea kuupata ugonjwa huu,”Alisema Michael D’ Hooghe.
Kwa Afrika tayari shirikisho la soka nchini Kenya FKF limemtangaza bingwa msimu wa 2019/20, kufuatia ligi ya nchi hiyo kusimama kwa muda mrefu huku kukiwa hakuna dalili za kurejea kwa wakati kama ilivyotarajiwa.
Klabu ya Gor Mahia imetangazwa kuwa bingwa wa ligi ya nchi hiyo, ikiwa imeshacheza michezo 23 na kujiusanyia alama 54.
Nchi nyingine barani Ulaya zilizochukua maamuzi ya kutangaza mabingwa licha ya ligi zao kufikia tamati ni ni Ubelgiji na Ufaransa, huku Uholanzi ikifuta ligi pasina kumtangaza bingwa.