Mshambuliaji wa pembeni kutoka nchini Argentina Angel Di Maria, jana aliwasalimu mashabiki wa klabu ya PSG ambao walikuwa kwenye uwanja wa nyumbani kushuhudia mchezo wa ligi daraja la kwanza nchini Ufaransa ambapo Paris St Germain walikua na shughuli ya kuwakabili Gazelec Ajaccio waliopanda daraja wakitokea ligi daraja la pili.

Kabla ya mchezo huo uliomalizika kwa PSG kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, Di Maria alijitokeza hadharani na kutumia nafasi ya klabu yake hiyo mpya kucheza mchezo wake wa kwanza nyumbani kwa kuwasalimu mashabiki ambao walikua na hamu ya kumuona tangu alipokamilisha uhamisho wake akitokea nchini England kwenye klabu ya Man Utd.

Mshambuliaji huyo alionyesha tabasamu la furaha sambamba na ishara ya upendo kupitia vidole vyake vya mkono, ambapo mara kadhaa amekua akifanya hivyo anapofunga bao akiwa na timu yake ya klabu ama timu yake ya taifa ya Argentina.

Hata hivyo Di Maria hakucheza mchezo huo kutokana na sababu ambazo hazikuanishwa na benchi la ufundi chini ya utawala wa Laurent Blanc  na alipojitokeza uwanjani alikua amevalia suti nyeusi.

Mabao ya PSG katika mchezo huo yalipachikwa wavuni na kiungo mfaransa Blaise Matuidi pamoja na beki kutoka nchini Brazil, Thiago Silva.

Ushindi huo umeiwezesha PSG kufikisha point 6 katika msimamo wa ligi daraja la kwanza nchini Ufaransa ambayo ilianza kutimua vumbi lake August 07.

Mzee Kingunge ‘Anena’ Kuhusu Taarifa Za Kuvuliwa Ukamanda Mkuu UVCCM
Barcelona Kulipiza Kisasi Leo?