Kiungo mchezaji ambaye ni raia wa Senegal, Mohamed Diame ametangaza kustaafu kuitumikia timu yake ya taifa kwa kuwasilisha ujumbe mzito kwa mashabiki wa soka.
Kupitia ujumbe huo, mchezaji huyo amesema haamini kama anastahili kuwa sehemu ya wachezaji walioipa mafanikio nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Diame mwenye umri wa miaka 29, ambaye kwa sasa anaitumikia klabu ya Newcastle Utd ya nchini England, ametangaza kuachana na Simba wa Teranga baada ya kucheza michezo 36 sambamba na michuano ya Olimpiki ya mwaka 2012 iliyofanyika jijini London.
“Ninaamini Senegal itaendelea kubaki salama na itakuwa na uwezo zaidi wa kupambana na timu nyingine barani Afrika na duniani kwa ujumla, wachezaji 23 ambao watateuliwa kwa ajili ya michuano yoyote ile watakuwa na uwezo mkubwa wa kulitetea taifa langu,” alisema Diame.
“Baada ya kujifikiria kwa kina, nimeamua kuachana na mpango wa kuitumikia timu yangu ya taifa, naamini wapo watakaokwazika na maamuzi haya, lakini sina budi kusema samahani kwao, inanibidi kuchukua maamuzi haya mazito,” aliongeza.
Diame amekuwa akitumika kama mchezaji wa akiba tangu kocha wa sasa wa Senegal Aliou Cisse, alipokabidhiwa kikosi mwezi Machi mwaka 2015.