Mwanamuziki Naseeb Abdul Juma Issack, maarufu Diamond Platnumz usiku wa kuamkia leo octoba 22, 2022, ametumbuiza katika tamasha la All Africa Festival.
Muda mfupi baada ya Tamasha hilo, kupitia ukurasa maalumu wa mtandao wa instagram wa WCB Wasafi waliweka video zenye kuonyesha tukio la kukutana kwa Diamond na msanii @mohamedramadanws kutoka nchini Misri ambao kwa pamoja wameingia studio kwa ajili ya kuandaa wimbo wa pamoja.
Mohamed Ramadan ni nani?
Kama hukuwa unamfahamu vizuri, Huyu ni msanii mkubwa na maarufu kutoka nchini Misri ambaye Afrika inamfahamu kama mfalme wa mtandao wa Youtube kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wafuatiliaji (Subscribers) wasiopungua 13.3 milioni na ndio msanii pekee kutoka barani afrika aliyefanikiwa kujipatia watazamaji zaidi ya 4.3 Bilioni kwenye mtandao huo maarufu Duniani.
Chanzo cha wawili hao kuingia studio pamoja ni baada ya kukutana Nchini Dubai ambapo wawili hao wote kwa pamoja walialikwa kutumbuiza kwenye tamasha maarufu nchini humo All Africa Festival 2021 lililofanyika usiku wa kuamkia leo October 22,2021.
Licha ya Mohamed kuwa msanii anayeongoza kwa namba kwenye mtandao wa Youtube barani Afrika, vitabu vya kumbukumbu vinatukumbusha kuwa msanii Diamond Platnumz ndio aliyekuwa msanii wa kwanza Afrika Mashariki na kati kufikisha kiwango cha watazamaji 1 Bilioni kwenye mtandao wa Youtube na anatambulika kama msanii mwenye wafuatiliaji (Subscribers) wengi zaidi kusini mwa Jangwa la Shahara.
Matarajio ya mashabiki wengi wa Wasanii hao ni kuwa wimbo wanaoandaa wasanii hao ukaweka rekodi ya kipekee kulingana na ukubwa na nguvu walizo nazo kwa kila mmoja na ukanda anaotokea.