Wakati ambapo makundi na timu zinazosapoti ushindani kati ya Diamond Platinumz na Ali Kiba yanazidi kuongeza wafuasi na kukua kila kukicha, waimbaji hao wameonekana kutosapoti harakati za makundi hayo.

Akiongea na XXL ya Clouds Fm, Diamond Platinumz alisema haungi mkono makundi yanayowashindanisha wasanii hao wa ndani na badala yake anawashauri watu wanaounda makundi hayo kufikiria katika kuwashindanisha wasanii wa ndani ya nchi na wale wa nje ya nchi ili kukuza muziki nchini.

Akitoa mfano, Diamond alisema ni bora watu hao wakamshindanisha yeye na Davido kisha wamsapoti yeye kwa nguvu hadi atakampomshinda kweli na baada ya hapo wamchukue msanii mwingine wa Tanzania na kumshindanisha na msanii mwingine mkubwa wa Nigeria, wamsapoti na amfunike kweli huyo wa Nigeria.

Alipoulizwa maoni yake kuhusu kampeni iliyoanzishwa na baadhi ya mashabiki wa Tanzania kwenye mitandao ya kijamii, kuwasapoti wasanii wa Nigeria dhidi ya Diamond katika vipengele vya tuzo za MTV/MAMA2015, alisema yeye haoni tatizo katika hilo kwa kuwa kila mtu ana haki na uhuru wa kumpigia kura msanii anaemtaka.

Mwimbaji huyo wa ‘Nana’ alisisitiza kuwa hajawahi kuwa na bifu na Ali Kiba anaeshindanishwa nae kila kukicha hasa kwenye mitandao ya kijamii.

Hivi karibuni, Ali Kiba alieleza kutofurahishwa na uwepo wa makundi yanayolenga kuleta uhasama kati ya wasanii hao wawili na kitendo cha baadhi ya makundi hayo kutaka kumuangusha msanii wa Tanzania na kumsapoti msanii wa nje ya nchi katika tuzo za kimataifa (MTV/MAMA2015).

Hivi karibuni, baadhi ya mashabiki walianzisha kampeni ya kuwasapoti wasanii wa Nigeria, Davido na Wizkid katika tuzo za MAMA2015 ili kumuangusha Diamond anaeshindana na wasanii hao katika tuzo hizo.

Al Shabaab yadai kuhusika na mauaji ya watu 14 Kenya
P Diddy amchapa 50 Cent fimbo ya kiutu-uzima