Mwanamuziki wa Bongo Fleva Diamond Platnumz amefanya ziara katika hospitali ya Amana iliyoko Ilala jijini Dar es salaam, ambapo amesababisha shughuli kusimame kwa muda.

Diamond amefanya ziara hiyo akisherehekea siku yake ya kuzaliwa leo Oktoba 2, 2017, na ametoa vifaa tiba vyenye thamani ya Sh4 milioni katika hospitali hiyo.

Akiwa hospitalini hapo wagonjwa na waliokuwa wakihudumiwa walitoka kwa ajili ya kumuona msanii huyo ambaye kwa sasa anatamba na ngoma yake ya mpya ya ‘Hallelujah’.

Diamond amesema alifikia uamuzi wa kwenda kwenye hospitali hiyo kwa kuwa ndiyo mahali alipozaliwa, amesema anajivunia kuwa na watu wazuri wa karibu ambao wanamshauri kuikumbuka  jamii inayomzunguka.

“Hospitali kuna mahitaji mengi nikaona kwa uwezo wangu mdogo namimi nishiriki kusaidia mahali nilipozaliwa siku ya leo ili nipate pia fursa ya kuwaona watoto waliozaliwa tarehe kama yangu, nafahamu kuna changamoto nyingi, niwasihi watu wengine waangalie ni namna gani wanaweza kusaidia,” amesema Diamond.

Akitoa neno kuhusu ziara hiyo, Kaimu mganga mkuu wa hospitali hiyo, Dkt. Shaany Mwaruka amempongeza Diamond kwa uamuzi huo na kutaka watu wengine waige mfano huo.

Amesema hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto ya vifaa tiba kutokana na idadi kubwa ya watu wanaowahudumia, hivyo amempongeza Diamond kwa kuwa mfano unaofaa kuigwa na wengine ukaleta manufaa katika jamii.

“Ungeweza kusherehekea siku yako ya kuzaliwa kwa kufanya chochote kile, lakini ukakumbuka mahali ulipozaliwa.” amesema Dkt. Mwaruka


Video: Lover Boy haukuwa wimbo wa Barnabas, D – Classic afunguka yaliyonyuma ya pazia kuhusu wimbo huo

Ofisi za Manji zafungwa na TRA, ni kuhusu deni la Sh. bilioni 12.2
Mchezaji jeuri arejeshwa kikosini Burkina Faso