Diamond Platinumz amefikishwa Mahakamani jijini Dar es Salaam akikabiliwa na mashtaka mawili ya madai ya uharibifu wa mali.
Mlalamika, Maulid Wandwi aliwasilisha mashtaka mahakamani akidai kuwa msanii huyo amefanya uharibifu kwenye nyumba yake aliyokuwa amempangisha kwa ajili ya studio katika eneo la Kijitonyama jijini humo.
Kwa mujibu wa malalamiko ya Wandwi, msanii huyo alifanya uharibifu unaogharimu Sh 337 Milioni. Diamond aliihamisha studio yake kutoka kwenye nyumba hiyo kwenda maeneo ya Mbezi. Kiasi hicho ni kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa na wasanifu majenzi.
Hata hivyo, Diamond hakuwa mahakamani hapo na aliwakilishwa na Wakili wake, Gerald Hamisi ambaye aliiambia Mahakama kuwa mteja wake yuko nje ya nchi na kutokana na hatari ya ugonjwa wa Corona atakuwa huko kwa kipindi kisichopungua siku 14.
Aidha, Wandwi pia amemshtaki Diamond Mahakamani akieleza kuwa anamdai kodi ya mwaka mmoja. Wakili wa mlalamikaji, Felix Buruda aliiambia Mahakama kuwa upande wa utetezi wanachofanya ni kutoa sababu ili kupoteza muda kwani wangeweza kuwasiliana na Diamond kwa barua pepe akiwa nje ya nchi.
Baada ya mvutano wa kisheria kati ya pande mbili, Hakimu wa Mahakama hiyo ya Ardhi, Laurent Wambili aliahirisha kesi hiyo hadi Jumatano, Machi 18, 2020.
Kesi hiyo ilianza kusomwa Mahakamani hapo Septemba 2019, na leo ilikuwa mara ya sita.