Diamond Platnumz na Nandy wameeleza kujutia kutumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kuweka au kurekodi video zinazowaonesha wakiwa faragha kwa nyakati tofauti na wapenzi wao.
Wasanii hao ambao wiki iliyopita walitiwa nguvuni na jeshi la polisi kwa kuvunja sheria na maadili, wameeleza majuto yao na kuiomba radhi Serikali na watanzania kwa ujumla baada ya kuhojiwa kwa takribani saa mbili na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), katika ofisi za makao makuu ya Mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuhojiwa, Diamond ameomba radhi kwa video alizoweka mitandaoni akiwa na msichana mwenye asili ya bara Asia na nyingine akiwa na mama mtoto wake, Hamisa Mobeto wakifanya yale yanayopaswa kufanywa faragha.
Diamond amesema kuwa atakuwa balozi na mfano kwa vijana kutumia vizuri mitandao ya kijamii na kutowavunja moyo viongozi wa Serikali wanaofanya juhudi za kuhakikisha muziki wa kizazi kipya unafika mbali.
“Wengi wanaamini kuwa mtandao ni kama chumba. Lakini wanashindwa kuelewa kwamba mtandao ni kama hadhara. Ina maana kwamba kitendo ambacho hupaswi kukifanya barabarani pale, kwenye mitandao hupaswi kukifanya,” alisema Diamond akirejea jinsi alivyofundwa na TCRA muda mfupi uliopita.
“Tunajua wasanii wana drama zao, wana kiki zao ambazo pengine walizoea kufanya miaka ya nyuma, lakini sasa kanuni zimebadilika… ikiwa Serikali inatukingia kifua na kutusapoti kuhakikisha muziki wetu unafika mbali, tukiwa tunaenda na hii njia ambayo sio nzuri pia tunakuwa tunawavunja moyo,” aliongeza.
Kwa upande wa Nandy, alisema kuwa amejifunza pamoja na mambo mengi kuwa sio tu kupost picha za faragha kwenye mitandao ni kosa bali pia hata kitendo cha kujipiga picha au kujirekodi video za matendo ya faragha au utupu ni kosa.