Mwanamuziki wa Bongo Flava wa Tanzania Naseeb Abdul, maarufu Diamond Platnumz ameikashifu serikali ya nchi hiyo kwa kuendelea kumdhalilisha licha ya kuwa mmoja wa walipaji ushuru wakubwa zaidi katika sanaa ya taifa hilo.

Msanii huyo ambaye anaendelea kuitangaza albamu yake ndogo kwa jina Fist of All, anadai kuwa wasanii wa lebo ya wasafi wamekuwa wakinyanyaswa na serikali kwa kutopewa uhuru wa kusafiri nje ya nchi mpaka ruhusa maalumu.

Akizungumza katika kipindi cha The Switch katika redio ya Wasafi FM, ambako ni mmoja wa walio na hisa nyingi zaidi, Diamond alifichua kuwa hana uhuru wa kuondoka nchini humo kama wasanii wengine.

Alidokeza kuwa ili kuondoka nchini humo lazima apate kibali kutoka kwa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) kila mara na akikosa yeye hukamatwa.

“Ninadhani ni wasanii tu waliosajiliwa Wasafi ambao hawaruhusiwi kuondoka nchini bila idhini ya serikali. Wakati wowote ninapofika katika uwanja wa ndege, ninakamatwa na kuzuiliwa kusafiri. Sijui mbona wanaendelea kunifanyia hili,” Diamond alimwabia mtangazaji Lil Ommy.

Diamond alisema kuwa ili kupata kibali hicho, yeye hulazimika kulipa shilingi pesa hata kama ni katika ziara ya kuwaona wanawe wawili walio nchini Afrika Kusini.

“Kila mara nikiuliza sababu, ninaambiwa kuwa lazima niwe na kibali kutoka kwa serikali kabla ya kuondoka nchini,” alisema.

Hata hivyo, BASATA kupitia kwa Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji Matiko Muniko, imekanusha madai hayo na kusema kuwa hakuna sheria ya mtu mmoja kwa kuwa wasanii wote wanaosafiri kwenda nje ya nchi wanatakiwa kutoa kiwango cha pesa ili kupata kibali kwa Tsh 50,000/=.

Bahati nasibu na mifuko inainua michezo Tanzania
Waziri Bashungwa awapa maagizo wakagizi halmashauri zote