Hatimaye Mlinda Lango wa Young Africans Djigui Diarra amefichua siri ya kufanya vizuri tangu alipotua klabuni hapo mwezi uliopita na kuonesha kiwango cha hali ya juu.
Mlinda Lango huyo kutoka nchini Mali amesema kujiamini na kujituma imekua silaha yake kubwa katika jukumu la kulinda lango ya klabu hiyo tangu alipowasili akitokea Stade Malien ya nchini kwao.
Amesema tangu alipotua Young Africans amekua mwenye furaha, baada ya kukuta mazingira mazuri ambayo pia yanamuwezesha kufanikisha kilichomleta nchini Tanzania.
Kuhusu kung’ara kwenye mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii dhidi ya Simba SC uliochezwa Jumamosi (Septamba 25), Diara amesema alifuata maelekezo ya makocha wake, pamoja na muunganiko mzuri wa safu yao ya ulinzi.
Diarra ni miongoni mwa nyota ambao walikuwa kwenye kiwango kikubwa kwenye mchezo huo na kuisaidia Young Africans kushinda taji la Ngao ya Jamii kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba SC, Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.
“Kwanza kabisa nashukuru sana kumaliza mechi salama na kufanikiwa kushinda taji la Ngao ya Jamii tena dhidi ya Simba, ulikuwa mchezo mzuri na ambao kila mmoja alipambana kwa jasho na damu kwa ajili ya timu.”
“Kuhusiana na kiwango changu naweza kusema siri kubwa ni kujituma mazoezini kufuata maelekezo ya mwalimu, na kushirikiana na wenzangu hasa wa safu ya ulinzi.”
Katika mchezo wa Jumamosi (Septamba 25), Diara alikuwa katika kiwango kikubwa ambapo alifanikiwa kuokoa mashuti matatu ya hatari yaliyolenga lango kati ya mashuti yote 15 ambayo yalipigwa na Simba katika mchezo huo.
Leo Jumatano (Septamba 29), Diara anatarajiwa kuanza langoni mwa Young Africans katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania bara msimu wa 2021/22, dhidi ya Kagera Sugar utakaopigwa Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba mkoani Kagera.