Mlinda Lango wa Young Africans Djigui Diara amesema ana imani kubwa klabu hiyo msimu huu 2021/22 itatwaa Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Young Africans inasaka taji la Ligi Kuu kwa msimu wa tano mfululizo, baada ya kulikosa kwa misimu minne, iliyoshuhudiwa Simba SC akitawala katika Ufalme wa Soka la Bongo.
Mlinda Lango huyo kutoka nchini Mali amesema, sababu kubwa inayompa jeuri ya kutamba kuwa na matumaini ya kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, ni kuwa na kikosi kizuri ambacho kina uwezo wa kushinda kila mchezo wa Ligi hiyo.
Amesema mbali na kuamini hivyo, bado yeye kama sehemu ya mchezo wa Young Africans, yupo tayari kuendelea kujitoa kwa namna yoyote ile, ili kufanikisha lengo la kuwa Mabingwa msimu huu 2021/22.
“Timu yetu ni nzuri nina asilimia zote lazima tutabeba ubingwa. Malengo yangu ni kuhakikisha inashinda kila mechi. Hilo nitafanya kwa kujitolea asilimia mia kwani ndio njia pekee ya kupata ubingwa. Hivyo nawaomba mashabiki wasihofu, tunabeba ubingwa.” Amesema Diara
Mpaka sasa Young Africans ndiyo timu pekee ambayo haijapoteza mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, zaidi ya kuambulia sare katika michezo mitatu dhidi ya Simba SC, Namungo FC na Mbeya City FC.
Klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 45 baada ya kushuka dimbani mara 17, huku Mabingwa watetezi Simba SC ikiwa kwenye nafasi ya pili kwa kufikisha alama 37.