Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wana-Diaspora kuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza Tanzania na kuainisha fursa zilizopo nchini, ikiwemo kuzisemea vizuri ili iwe fursa ya kupata wawekezaji ambao watakuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali na ikibidi wafanye ubia na Watanzania.
Waziri Mkuu, ambaye yuko Tokyo, Japan ametoa wito huo hii leo Septemba 28, 2022 alipokutana na Jumuiya ya Watanzania waishio Japan Tanzanite, iliyo na wanachama wafanyakazi waajiriwa, waliojiajiri na wanafunzi.
Amesema, “Wana-Diaspora tafuteni marafiki wa kwenda kuwekeza nyumbani kwenye sekta mbalimbali kama utalii, madini, viwanda. Tunawategemea ninyi katika kupata hawa wawekezaji ambao ni makini kwa sababu ninyi mnaishi nao, mnawajua zaidi.”
Aidha amewataka kukitumia Kiswahili kama njia ya kukuza ajira kwani nchi nyingine zimeona fursa hiyo na zimeamua kukiweka kwenye mitaala yao (syllabus) huku akitumia fursa hiyo kueleza mafanikio yaliyofikiwa na Serikali ya awamu ya sita ikiwemo uboreshaji sekta za elimu, afya, maji, nishati, usafiri na usafirishaji, miundombinu ya barabara na reli.
Akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Japan, Frank Semaganga, amesema jumuiya hiyo yenye wanachama 400, ilianzishwa ili waweze kusaidiana, kuleta mshikamano na kuitangaza Tanzania.
Aidha, ameiomba Serikali iangalie uwezekano kuboresha mifumo ya uendeshaji kwenye Soko la Hisa (DSE) ili wana-Diaspora waweze kuwekeza kwa kununua hatifungani pindi zinapotangazwa.
Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi wanaosoma Japan (TSJ), Eunice Likotiko aliiomba Serikali iangalie namna ya kutumia vizuri ujuzi wa Watanzania wanaosoma nje ya nchi pindi wanapohitimu na kurejea nchini.
Mkutano huo, ulihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassoro Mbarouk na Balozi wa Tanzania nchini Japan, Balozi Baraka Luvanda.