Beki wa Kulia Dickson Mhilu, amekanusha taarifa za kuwa mbioni kuikacha Kagera Sugar, baada ya kuhusishwa na taarifa za kuwaniwa na klabu kadhaa za Ligi Kuu Tanzania Bara kuelekea msimu ujao wa 2022/23.
Mhilu mabaye ni Mchezaji Bora Chipukizi wa Ligi Kuu msimu wa 2021/22, amevunja ukimya huo, baada ya kutakiwa kuweka wazi mipango yake kwa msimu ujao.
Kinda hilo limesema bado lipo Kagera Sugar kwa mujibu wa mkataba wa miaka miwili aliousaini siku za karibuni, hivyo kama itatokea anaondoka basi itatokana na Baraka kutoka kwa Viongozi wake.
Amesema anasikia taarifa za kuwania na klabu kadhaa za Ligi Kuu, lakini ukweli ni kwamba hajawahi kuzungumza na Kiongozi yoyote, na hakuna ofa yoyote iliyowasilishwa kwenye klabu ya Kagera Sugar.
“Uongozi uliniongeza mkataba wa miaka miwili hivyo mimi ni mali halali ya Kagera Sugar, ikitokea ninaondoka hapa basi nitaondoka kwa Baraka za Viongozi na klabu yangu.”
“Nasikia taarifa za kuwania na klabu kadhaa za Ligi Kuu, lakini ukweli ni kwamba hakuna Kiongozi yoyote aliyewasiliana nami, wala Uongozi wangu au Uongozi wa klabu,”
“Kama kuna yoyote anahitaji huduma yangu anapaswa kuonana na Uongozi wa Kagera Sugar, baada ya hapo mambo mengine kama yatakaa sawa nikakuwa tayari kuondoka, lakini sio kwa mimi kujiamulia kama nipo huru.” Amesema mchezaji huyo ambaye ni ndugu wa Kiungo Mshambuliaji wa Simba SC Yusuph Mhilu