Gwiji wa soka kutoka nchini nchini Ujerumani Didi Hamann ametoa mtazamo wake kuelekea mchezo wa mahasimu wa jadi katika ligi ya England Liverpool na Man utd, ambao utachezwa mwishoni mwa juma hili.
Hamann ambaye aliwahi kuitumikia Liverpool katika nafasi ya kiungo kuanzia 1999–2006, amesema anaipa nafasi kubwa Man Utd kuibuka na ushindi siku hiyo, kwa kuamini watakua na bahati ya kipekee.
Amesema Liverpool itakwenda katika mchezo huo ikiwa na mapungufu makubwa katika safu ya ushambuliaji, hali ambayo huenda ikapunguza kasi ya kulisakama lango la Man Utd.
Kutokuwepo kwa Sadio Mane ambaye amerejea barani Afrika kwa ajili ya fainali za AFCON 2017, kunamuaminisha itakua sababu ya Liverpool kushindwa kufikia lengo la kumaliza dakika 90 wakiwa na point tatu mkononi.
“United watakua na bahati ya kupambana wakati wote kutokana na udhaifu ambao ninauona ndani ya kikosi cha Liverpool. Mane amekua na kashkash za kuongeza mashambulizi katika lango la timu pinzani,”
“Man Utd wamekua na matokeo mazuri katika siku za karibuni, na ninaamini jambo hili litawasaidia kwa kiasi kikubwa, kwa kupambana wakati wote huku wakijiamini.” Alisema Hamann alipohojiwa na Sky Sports.