Uongozi wa shirikisho la soka nchini Ufaransa (FFF) umemuhakikishia kocha mkuu wa timu ya taifa hilo Didier Deschamps, kutokua na woga wa kutimuliwa kazi, endapo hali itakua tofauti katika michezo ya hatua ya mtoano katika fainali za kombe la dunia, inayoanza leo.
Uongozi wa FFF umesema una imani kubwa na Deschamps, kutokana na kazi nzuri aliyoifanya tangu alipoajiriwa mwaka 2012, na mpaka sasa wameridhishwa na kiwango cha timu yao ambayo itacheza mchezo wa hatua ya 16 bora dhidi ya Argentina baadae hii leo.
Deschamps, ambaye alikiongoza kikosi cha Ufaransa kama nahodha wakati wa fainali za kombe la dunia mwaka 1998, tayari alikua ameshaanza kuwekewa vikwazo na wadau wa soka nchini kwao, ambao wamekua wakihoji aina ya soka linalocheza na kikosi chao.
Wadau hao wakaenda mbali zaidi na kumpendekeza aliyekua meneja wa klabu bingwa barani Ulaya Real Madrid Zinedine Zidane, kupewa kikosi cha Ufaransa, ili alete mabadiliko kama ilivyokua wakati akikabidhiwa kikosi cha The Merrengues.
“Tumeshasaini mkataba mpya na Deschamps ambao utafikia kikomo mwaka 2022, tutahakikisha tunaheshimu vipengele vya mkataba huo kwa kumpa nafasi ya kufanya kazi yake kwa ufasaha,” imeeleza taarifa iliyotolewa na FFF.
Mchezo kati ya Ufaransa na Argentina utakaochezwa baadae hii leo, utakua wa 80 kwa kocha huyo, na ataweka rekodi ya kuwa kocha aliyedumu kwa muda mrefu, baada ya Raymond Domenech aliyeshuhudia michezo 79 wakati wa utawala wake.