Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ufaransa Didier Deschamps amesema anaamini siku moja Zinedine Zidane atakuwa kocha wa timu hiyo ya taifa lake.
Deschamps ambaye mkataba wake wa kuifundisha timu hiyo unamalizika 2020, amesema anaamini Zidane ananafasi kubwa ya kuchukua mikoba yake mara baada ya kuondoka Real Madrid.
Kocha huyo ambaye alikuwa na Zidane kwenye kikosi cha ufaransa kilichoshinda kombe la Dunia mwaka 1998 kwenye ardhi yake ya nyumbani, amesema atafurahi endapo atamuachia mikoba ya kuifundisha timu ya taifa.
“Namuachia raisi wa shirikisho la soka la Ufaransa, Noel Le Graet, sifahamu Zidane ameamua nini nadhani kwa sasa anataka kufurahia mafanikio na familia na watu anaowapenda’’ Deschamps amewaambia waandishi wa habari.
‘’Nadhani baada ya hapo atakuwa kocha wa Ufaransa siku moja, ni lini? Siwezi kujua ‘’ ameongeza Deschamps.
Aidha, kocha huyo amesema anaheshimu maamuzi ya Zidane kwa kuwa mafanikio aliyoyapata kwenye miaka mitatu iliyopita ndani ya Real Madrid ni yakujivunia kwake binafsi na klabu kwa ujumla.
Zinedine Zidane ametangaza kuacha kuifundisha Real Madrid wiki hii siku chache baada ya kuiongoza kuchukua kombe la klabu bingwa barani ulaya kwa mara ya tatu mfululizo amesema lengo lake ni kupumzika, akifata nyayo za aliyekuwa kocha wa Barcelona Pep Guardiola.