Aliyekua mshambuliji wa klabu ya Chelsea ya nchini England Didier Drogba ametangaza rasmi kustaafu kusakata kabumbu baada ya kudumu katika soka la ushindani kwa takriban miaka 20.
Mshambuliaji huyo raia wa Ivory Coast mwenye umri wa miaka 40 ameitumikia Chelsea kwa vipindi viwili tofauti, mwaka 2004 hadi 2012 na msimu wa mwaka 2014 -2015.
Akiwa katika klabu hiyo ya London, Drogba amecheza mechi 381 akiifungia magoli 164 huku akifanikiwa kushinda mataji manne la Ligi Kuu nchini England (EPL), mataji manne ya Kombe la FA, mataji matatu ya Kombe la Ligi na kombe moja la Mabingwa Ulaya mwaka 2012.
Kabla ya kustaafu, Drogba alikuwa akiitumikia klabu ya Phoenix Rising ya nchini Marekani tangu mwaka 2017, yeye akiwa ni mchezaji na mmiliki mwenza.
Baada ya miaka 20, nimeamua kutundika daluga… Ni vema kupumzika na kusaidia kuendeleza vipaji vipya. Nimejifunza mambo mengi kwenye soka na ninafikiri ni vema sasa kujitoa kwaajili ya kuusaidia mchezo huo”, amesema Drogba.
Akiwa kijana, Drogba alipitia vilabu mbalimbali ikiwemo Tourcoing alikoanzia kabumbu mwaka 1988 kabla ya kujiunga rasmi na timu ya Le Mans ya Ufaransa mwaka 1997 ambako mwaka 1998 alihamishiwa timu ya wakubwa na ndiyo ukawa mwanzo wake wa soka la ushindani.
Alijiunga na Chelsea mwaka 2004 akitokea Marseille kwa ada ya paund milioni 24 na alipoanchana na Chelsea mwaka 2012 alikimbilia nchini China kwenye klabu ya Shanghai Shenhua kabla ya kujiunga na Galatasaray mwaka 2013 na kisha kurejea Chelsea mwaka 2014 alipodumu kwa mwaka mmoja.
Hadi anastaafu ameitumikia timu yake ya Taifa ya Ivory Coast kwa takriban miaka 12, kuanzia 2002 hadi 2014 akiichezea michezo 104 na kufunga mabao 65.