Aliyewahia kuwa Kocha wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Didier Gomes ameitakia kila la kheri timu hiyo kuelekea mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo huo utakaounguruma Jumapili (April 17) Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo wakiwa na matarajio makubwa ya ushindi kwa timu yao.
Gomes ambaye aliondoka Simba SC baada ya timu hiyo kutolewa kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa kufungwa na Jwaneng Galaxy ya Botswana mabao 3-1, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam mwezi Oktoba mwaka 2021, amesema endapo Simba SC itacheza vizuri dhidi ya Orlando Pirates keshokutwa Jumapili (April 17), itakua na nafasi kubwa ya kushinda.
Amesema anafahamu wachezaji wa Simba SC wanapokua na jukumu kama hilo wanavyokua, hivyo amewatakia kila la kheri kwa kuamini uchu wa mafanikio walionao utakua msukumo mkubwa kwao kupambana, ili kupata matokeo mazuri kwenye Uwanja wa nyumbani.
“Kama Simba itacheza vizuri, inaweza kufika hatua ya Nusu Fainali, najua tabia za wachezaji wa Simba SC wanapokua katika mchezo mgumu kama huu, huwa wanaamini kuna jambo kubwa linalowasukuma ili wafanye vizuri.”
“Naamini katika kipindi hiki hali hiyo imewajaa vifuani mwao, binafsi ninawatakia kila la kheri ili waweze kuifunga Orlando Pirates na kusonga mbele katika hatua ya Nusu Fainali.” Amesema Kocha huyo kutoka nchini Ufaransa.
Mara baada ya kuondoka Simba SC Didier Gomes aliajiriwa na Shirikisho la Soka nchini Mauritania kama Kocha Mkuu wa timu ya taifa hilo, lakini baada ya Fainali za AFCON 2021 zilizochezwa mapema mwaka huu nchini Cameroon, alisitishiwa mkataba wake kufuatia kushindwa kufikia malengo aliyowekewa.