Joto la mchezo wa mzunguuko wa tano wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Hatua ya Makundi kati ya Simba SC dhidi ya AS Vita Club linaendelea kupanda, huku kila upande ukiamini utaokota alama tatu muhimu jijini Dar es salaam.

Simba SC itakuwa wenyeji wa mchezo huo Uwanja wa Benjamin Mkapa mapema mwezi ujao (April 03), huku ikihitaji alama moja tu! kufuzu hatua ya Robo Fainali ikitokea ‘Kundi A’ la michuano hiyo lenye timu nyingine kama Al Ahly ya Misri na Al Merrikh ya Sudan.

Kocha Mkuu wa Simba SC Didier Gomes ametamba kuwa anaamini kikosi chake kitaweza kuibuka na ushindi katika mchezo huo, ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabik na wanachama wa Mabingwa hao wa Tanzania Bara.

“Tunajua tuna mchezo mgumu mbele yetu dhidi ya AS Vita, lakini nina imani kubwa vijana wangu watapambana ili kuweza kupata alama tatu muhimu hapa nyumbani.” amesema Gomes.

Kwa upande wa AS Vita watahitaji kuutumia mchezo huo kama sehemu ya kulipa kisasi cha kufungwa nyumbani kwenye mchezo wa mzunguuko wa kwanza, ambapo Simba waliibuka na ushindi wa 1-0, mjini Kinshasa, DR Congo.

Hata hivyo hii haitokua mara ya kwanza kwa AS Vita kucheza Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam, kwani kamaitakumbukwa vyema timu hiyo inayonolewa na Florent Ibenge ilipoteza mbele ya Simba SC msimu wa 2018/19 kwa kufungwa 2-1, na kutupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya Makundi.

Mpaka sasa Simba SC inaongoza msimamo wa ‘Kundi A’ la michuano hiyo wakiwa wamejikusanyia alama 10, wakifuatiwa na mabingwa watetezi wa michuano hiyo Al Ahly wenye alama 7, AS Vita wao wako kwenye nafasi ya tatu na alama 4, huku Al Merrikh ya Sudani wao wakiburuza mkia na alama 1.

Mamia washiriki mazishi ya ndugu wanaodaiwa kufariki kwa kukanyagwa
Magufuli alikuwa na maono makubwa- Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar